Maisha Ya Mke wa Deo Filikunjombe Baada ya Miaka Miwili ya Kifo Cha Mumewe..!!!


MAMA shujaa! Ikiwa imebaki miezi minne na siku kadhaa itimie miaka miwili kutokea kwa kifo cha aliyekuwa kada muaminifu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mbunge wa Jimbo la Ludewa mkoani Njombe, marehemu Deo Haule Filikunjombe, mkewe Sarah Filikunjombe (Pichani) amethibitisha ushujaa kwa kuendelea kupambana na changamoto za kimaisha na kufikia vilele mbalimbali vya mafanikio, Ijumaa limemfungia kazi.
Mwishoni mwa wiki iliyopita na mwanzoni mwa wiki hii, kwa siku tatu tofauti, waandishi wetu walijipa kazi ya ziada ya kumtafuta Sarah ili kujua nini kimeendelea katika maisha yake baada ya kuondoka kwa mumewe ambapo walibaini mambo mengi mazuri yenye kutia moyo, ambayo mama huyu licha ya kuonekana sistaduu, ameyafanya kwa ujasiri wa kipekee.

IJUMAA NYUMBANI KWAKE

Hatimaye Jumanne mchana, gazeti hili lilifika nyumbani kwake, Kijichi Mbagala jijini Dar na kufanya naye mahojiano ambapo alitoa ushirikiano wa kutosha na kufunguka mengi juu maisha yake tangu kuondokewa na mumewe.

BAADA YA KIFO CHA MUMEWE

“Kufiwa ni kovu la milele maishani, kifo cha mume wangu kiliniumiza sana na hata sasa sijapona jereha hilo, nililia, nilihuzunika na bado nahuzunika lakini ilikuwa lazima maisha yaendelee. Aliniacha na watoto ambao bado ni wadogo hivyo wanahitaji uangalizi wa hali ya juu, kwa hiyo ilinibidi nijipange upya namna ya kuwatunza,” alisema Sarah na kuongeza; “Ukiondoa nyumba na miradi mingine, mume wangu aliacha Kampuni ya Jumbo Camera House inayojishughulisha na uuzaji wa kamera za kisasa, iliyopo Posta Mpya, kwenye Jengo la Benjamin Mkapa, lakini sikutaka kabisa kutegemea kitu hicho pekee, niliamua kuangalia njia nyingine za kuingiza kipato ili nikikusanya huku na huku, maisha yanasonga kwa wepesi.

“Hivyo, nilianza kujishughulisha na kilimo na ufugaji ambapo nafuga kuku wa kisasa na pia nina mabwawa ya kufuga samaki aina ya kambale, vyote hivyo viko wilayani Mkuranga Mkoa wa Pwani, pia nimewekeza kwenye vinywaji ambapo nimefungua baa iliyopo Vianzi hukohuko Mkuranga na vilevile niko kwenye hatua ya mwisho kukamilisha mradi wa kuuza unga wa sembe ambao nitakuwa naufunga kwenye viroba, yote hayo yako chini ya Kampuni ya Tripple L, ambayo inawakilisha majina ya wanangu wapendwa watatu, Lee, Levis na Larry ambapo hata nembo ya viroba vya unga itakuwa na picha yetu wote wanne,” alisema Sarah.

MARAFIKI WAPO PAMOJA NAYE?

“Idadi imepungua kwa kweli, hata wale marafiki waliokuwa karibu na mume wangu hawana tena ule ukaribu kama ilivyokuwa zamani, lakini huwezi kulaumu maana majukumu yanabana na kila mtu anapambana kukimbiza ndoto zake maishani.

“Hata marafiki zangu wamebaki wachache sana, wengi walidhani ningekuwa tegemezi na niseme bila kuficha walikuwa karibu na mimi kipindi mume wangu akiwa hai, wakitarajia msaada wa haraka . Sasa mambo yamebadilika, ingawa mimi nipo na ninapigana na maisha, simtegemei mtu zaidi ya Mungu na wale wanaokuwa karibu yangu maana sasa nina marafiki wapya kabisa,” alisema Sarah.

KUNA HILI LA MADENI “Katika mzunguko wa kutafuta mafanikio maishani, hususan kwa wafanyabiashara jambo la madeni halikwepeki, iwe kudai au kudaiwa. Sisi tunadaiwa na duka moja kule Dubai, wakati mume wangu akiwa hai, alikopa mzigo na alifariki tukiwa bado hatujakamilisha lakini Mungu yu mwema ulipaji utakamilika na pia tuna pesa tunadai, siwezi kusema ni wapi lakini ieleweke tu kwamba kuna mahali tunadai na vilevile matarajio ya kulipwa ni makubwa,” alisema.

SUALA LA MIRATHI LIKOJE?

“Kuna watu wanashughulikia jambo hilo, hivyo siwezi kulisemea chochote.”

ANASAIDIA NYUMBANI KWAO?

“Japo si kwa haraka kama ilivyokuwa zamani, sasa hivi wakihitaji msaada kutoka kwangu, lazima niwaambie wasubiri kwanza nijikusanye au kuangalia kilichopo kwa wakati huo, unajua kwenye familia yetu ni mimi na dada yangu ndiyo tumejaaliwa kuwa na unafuu wa kimaisha hivyo familia yetu ni ya kawaida sana kwa maana ya kipato,” alisema Sarah.

MSAADA KWA WANAWAKE WENZAKE


“Sitaki kujisifia juu ya hilo, lakini kwa kidogo nilichojaaliwa kwa maana ya mawazo ya kimaisha, huwa nashirikiana sana na wanawake wenzangu, hususan wajane kama nilivyo, kuna kipindi nilikuwa naendesha mafunzo ya namna ya kufuga samaki bure na elimu ya kufungua miradi mbalimbali, sikutaka malipo yoyote na hata sasa huwa nawafundisha, nikitarajia malipo kutoka kwa Mungu,” alisema Sarah.

VIPI KUHUSU MRITHI WA DEO?

“Hapana, kwa sasa nimeelekeza nguvu na akili yangu yote kwa wanangu, nawapenda mno, zaidi ya neno lenyewe na hata wao wanajua kuwa nawapenda, napambana kuhakikisha wanapata mahitaji yao yote kwa wakati, sitaki kujiingiza kwenye mambo ya kuwekeana msongo wa mawazo na mwanaume mwingine, pia hayupo wa kuziba pengo la marehemu mume wangu mpendwa, ameacha nembo ya milele maishani mwangu, kwa hiyo siwezi kuwaza kuwa na mtu kwa sasa,” alisema.

NENO LAKE KWA WAJANE NA WANAWAKE KWA UJUMLA

“Kufiwa ni jambo moja, lakini haipaswi kulia tu
bila kutenda jambo. Kama nilivyosema mwanzoni, kovu la kufiwa lina maumivu ya kuvuka kiwango cha kutamkwa, lakini lazima mwanamke asimame na kupambana na maisha, wapo wanawake wengi walifiwa na wanaume zao na kuwaacha mikono mitupu kabisa, wakati mwingine kunyang’anywa kila kilichokuwepo na baadhi ya ndugu, lakini leo hii wamesimama na kufanikiwa zaidi ya ilivyokuwa awali. “Nguvu ya mwanamke ni kubwa, mwanamke ni kiumbe wa pekee mno akiamua kufanya jambo kwa kuielekeza akili na nguvu yote kwenye jambo husika, lazima lifanikiwe ndiyo maana kuna ule msemo kwamba nyuma ya mafanikio ya kila mwanaume kuna mwanamke, hivyo sisi ni Generation point (chanzo cha uzalishaji) ya mafanikio, Mungu ameweka nguvu kubwa mno maishani mwetu, wanawake tuamke na tuzidi kupambana huku tukimuweka Mungu kama nguzo muhimu maishani,” alisema Sarah.

ANAO MPANGO WA KUJITOSA KWENYE SIASA?

“Sifikirii, nina mambo mengi sana kuhusu maisha na siasa inahitaji muda wa kutosha katika kuwahudumia wananchi, nilikuwa naona wakati wa mume wangu, jinsi alivyokuwa akijitoa kwenye siasa na wakati mwingine zaidi ya ilivyokuwa kwa familia, kwa hiyo sina wito wa siasa, mimi napambana na maisha tu,” alisema Sarah Filikunjombe katika mahojiano hayo maalum.

NI MAUMIVU KUKUMBUKA, LAKINI TURUDI NYUMA KIDOGO

Marehemu Deo Haule Filikunjombe alifariki dunia Oktoba 15, mwaka 2015 wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu, katika ajali ya chopa ilikuwa na usajili namba 5Y-DKK ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Selous, ambapo watu wengine watatu walifariki, akiwemo rubani William Silaa, aliyekuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime mkoani Mara, Egdi Mkwera na aliyekuwa mtumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, Vitalis Blanko Haule

Related Posts

Post a Comment