WAVUVI 53 WAOKOLEWA BAADA YA MASHUA KUZAMA BAHARINI ZANZIBAR

Wavuvi 53 waokolewa baada ya mashua yao ya uvuvi kuzama nje kidogo ya pwani ya Zanzibar.
Msemaji wa Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Zanzibar, Bi Shekha Ahmed Mohamed alieleza kuwa shughuli ya kuwatafuta na kuwaokoa wahanga wa ajali hiyo iliyofanywa na tasisi ya uokozi imefanikiwa kuwaokoa wavuvi wote wakiwa hai, ambapo 44 waliokolewa mapema na wengine 9 kuokolewa baada ya kukaa baharini kwa zaidi ya saa 24.
“Watatu kati ya hao hawakuwa na hali nzuri na walifikishwa katika hospitali ya Kivunge kwa ajili ya matibabu” alisema
Kaimu Mkurugenzi wa kitengo cha Ujasusi, Makarani Mohamed alisema kuwa chanzo cha ajali hiyo kinasadikika kuwa ni hali mbaya ya upepo na mawimbi makali yaliyokuwa baharini kwa wakati huo.
“Tunafahamu kuwa ajali hiyo ilisababshwa na upepo na mawimbi makali yaliyosababisha mashua hiyo kuzama”
Mvuvi mmoja aliyenusurika katika ajali hiyo aliwaambia waokoaji kuwa mashua hiyo iliondoka jana jioni na watu takriban 53 kwenda kuvua samaki wakati hali ya bahari ikiwa shwari na tulivu. Lakini hali ya hewa ilibadilika na kusababisha mawimbi makali baharini na kuongeza kuwa tokea ajali hiyo itokee hajamwona mwenzake hata mmoja.
Mkuu wa kituo cha Mamlaka ya Usafiri Baharini Mkoa wa Kaskazini Unguja, Pandu Juma Pandu amesema kuwa wako katika mchakato wa kuvisajili vyombo vya usafiri wa baharini ili kujua uzima na uimara wake, shughuli ambayo ilikuwa ikifanywa na idara ya uvuvi hapo awali.
Hata hivyo uvuvi katika kisiwa cha Zanzibar ndiyo shughuli kuu ya wakazi wa huko na mashua nyingi huwa katika hali ya uchakavu jambo ambalo ni hatarishi kwa usalama wa wavuvi wawapo baharini.

from Blogger http://ift.tt/2nHzUBD
via IFTTT

from WordPress http://ift.tt/2oMvsmW
via IFTTT

from Blogger http://ift.tt/2ng587I
via IFTTT